Ras Inno Nganyagwa Kutambulisha rasmi bendi yake
MWANAMUZIKI
nguli wa miondoko ya reggae hapa nchini, Ras Inno Nganyagwa, anatarajia kuitambulisha
rasmi bendi yake katika onesho mahsusi linalotarajiwa kufanyika katikati ya
mwezi ujao jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na gazeti hili, Ras Inno alisema kwamba huo ni mwanzo wa kutimiza mikakati yake
ya harakati za kurudi kwenye fani baada ya kujiweka pembeni kwa muda mrefu.
Alisema
kwamba, onesho hilo licha ya kuitambulisha bendi hiyo, lakini pia litakuwa
mahsusi kwa ajili ujio wake mpya wenye mbinu za kisasa za kiweledi za kufanya
kazi.
Nguli
huyo ambaye pia ni mtafiti wa masuala mbalimbali ya kijamii na mwandishi maarufu
wa safu mbalimbali katika magazeti ya hapa nchini, alibainisha kuwa baada ya
kuwa nje ya ulingo kwa muda mrefu.
“Nimeamua
kurudi rasmi kivingine kwenye fani baada ya kuusoma muziki wa reggae nikiwa pembeni
na kubaini mapungufu kadhaa niliyotathmini, hivyo nimebuni mikakati mbadala tofauti
ya namna bora ya kurudi jukwaani kwa dhamira ya kuipaisha reggae, pia kukonga
nyoyo za mashabiki wake ambao hawajamuona jukwaani kwa muda mrefu,” alisema.
Akifafanua
zaidi alisema kuwa licha ya kuitambulisha bendi yake ya kudumu atakayokuwa
akitumbuiza nayo, tofauti na zamani ambapo alitumbuiza zaidi kama mwanamuziki huru
anayepiga na kundi la wapiga vyombo bila jina rasmi la bendi.
Onesho
hilo mahsusi pia litakuwa maalum katika kuitambulisha taasisi yake aliyoiunda
itakayosimamia kazi zake ikiwemo bendi, pamoja na miradi aliyoibuni yenye lengo
la kuupromoti muziki wa reggae ili kuhakikisha vijana wengi wanavutika na
kujitosa kwenye miondoko hiyo, ili kupanua wigo wa idadi ya wanamuziki wa
reggae kwa kuibua vipaji vipya.
Alisema
onesho hilo litakalohudhuriwa na wadau wa muziki watakaoalikwa ambao taasisi
yake inatarajia kushirikiana nao siku za usoni, litatumika pia kuitambulisha
rasmi albamu yake mpya ya nne aliyoirekodia katika studio za Soundcrafters
zilizopo Temeke hapa jijini, anayotarajia kuizindua hivi karibuni.
“Katika
onesho hilo nitapiga nyimbo zangu zilizonipatia umaarufu miaka ya nyuma ukiwemo
wimbo wa ‘Gila’ kutoka albamu ya Money-Pesa (1994), pamoja na nyimbo nyingine
kutoka albamu zangu mbili zilizofuata na nyimbo mpya kutoka katika albamu mpya
ya ‘Kwa Nini’.”
Utambulisho
huo ni mwanzo wa maandalizi ya uzinduzi utakaofuatiwa na ziara ya maonesho
yasiyopungua kumi katika awamu ya kwanza, itakayoanzia hapa jijini kabla ya
kuelekea nyanda za juu Kusini na baadaye awamu ya pili itahusisha kanda ya
Kaskazini na ziwa katika mfululizo wa maonesho ya kupromoti albamu yake mpya na
muziki wa reggae kwa ujumla.
Katika
onesho la utambulisho atasindikizwa na kundi la Kizazi Kipya cha Reggae, bendi
ya Fimbo inayopiga miondoko ya asili, mwimbaji wa muziki wa gospo Mrs Annette
Mwasambogo na Dj maarufu wa disco la reggae hapa nchini Aluta Warioba kutoka
redio ya Times FM.
No comments:
Post a Comment