Monday, April 29, 2013

Sasa Bendi ya Ras Inno yakamilika, kuzinduli wa mwezi ujao




HATIMAYE bendi ya nguli wa muziki wa reggae nchini, Ras Inno Nganyagwa imekamilika na anatarajia kuizindua rasmi mwezi ujao jijini Dar es Salaam.

Ras Inno ambaye ni mshindi wa tuzo nne za mwanamuziki bora wa reggae Tanzania, amesema bendi yake hiyo ina wanamuziki 11 na itazinduliwa katika hafla maalumu katika ukumbi utakaotangazwa hapo baadaye.

Amasema nia ya kuanzisha bendi hiyo ni kuwa na ufanisi bora zaidi wa kufanya kazi zake za muziki, kwani bendi ya kudumu na wanamuziki wa kudumu hujenga ‘patern’ ambayo ni sawa na wachezaji waliozoeana uwanjani.

“Hiyo hulinda ladha ya nyimbo husika kutobadilika kila show, pia uhakika wa kufanya kazi njema nje ya nchi. Lakini pia kuwa na bendi huhakikisha upatikanaji wa tija ya kudumu, tofauti na ukiwa ‘solo’ tu bila jina la bendi kazi huja kwa misimu kutokana na mazoea ya hapa kwetu Bongo,” amesema.

Amesema bandi hiyo ni mojawapo ya miradi iliyo chini ya usimamizi wa taasisi yake mahsusi ya kuupromoti muziki wa reggae, kwa ushirikiano na wadau wengine miongoni wa mitindo mingine kwa kuzingatia weledi.

“Taasisi inaitwa Reggae Production House ambayo itahakikisha uzalishwaji wa vipaji vipya vya vijana wanaotaka kuingia kwenye reggae, kwa kufuata njia sahihi itakayowajenga kuwa wanamuziki bora wa reggae nchini watakaoweza kufanya kazi kimataifa.

“Dhima nzima ni kuufufua muziki wa reggae hapa nchini si kwa kuwa umekufa, la hasha, ila kuna mazingira yanayoufanya muziki huu uonekane kama haupo, lakini mahitaji yapo na mashabiki wana hamu kubwa nao.”

Aidha ameongeza kusema kwamba, ukimya wake wa muda mrefu una sababu kadhaa zikiwemo za kibinafsi kimaisha, lakini muda aliokuwa nje ya ulingo, ameyasoma vyema mazingira yanayoukabili mtindo wa reggae hivyo naamini ana dozi ya kuutibu.

“Ninayodhamiria kuyafanya kupitia taasisi yangu na vitengo vyake ikiwemo bendi, havijapata kuonekana kabla kwenye tasnia ya reggae hapa nchini. Hivyo basi naamini mwanzo huu wa mapinduzi, utaungwa mkono na wadau wote wenye mapenzi mema.”

reggeaproduction



Ras Inno Nganyagwa Kutambulisha rasmi bendi yake

MWANAMUZIKI nguli wa miondoko ya reggae hapa nchini, Ras Inno Nganyagwa, anatarajia kuitambulisha rasmi bendi yake katika onesho mahsusi linalotarajiwa kufanyika katikati ya mwezi ujao jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili, Ras Inno alisema kwamba huo ni mwanzo wa kutimiza mikakati yake ya harakati za kurudi kwenye fani baada ya kujiweka pembeni kwa muda mrefu.

Alisema kwamba, onesho hilo licha ya kuitambulisha bendi hiyo, lakini pia litakuwa mahsusi kwa ajili ujio wake mpya wenye mbinu za kisasa za kiweledi za kufanya kazi.

Nguli huyo ambaye pia ni mtafiti wa masuala mbalimbali ya kijamii na mwandishi maarufu wa safu mbalimbali katika magazeti ya hapa nchini, alibainisha kuwa baada ya kuwa nje ya ulingo kwa muda mrefu.

“Nimeamua kurudi rasmi kivingine kwenye fani baada ya kuusoma muziki wa reggae nikiwa pembeni na kubaini mapungufu kadhaa niliyotathmini, hivyo nimebuni mikakati mbadala tofauti ya namna bora ya kurudi jukwaani kwa dhamira ya kuipaisha reggae, pia kukonga nyoyo za mashabiki wake ambao hawajamuona jukwaani kwa muda mrefu,” alisema.

Akifafanua zaidi alisema kuwa licha ya kuitambulisha bendi yake ya kudumu atakayokuwa akitumbuiza nayo, tofauti na zamani ambapo alitumbuiza zaidi kama mwanamuziki huru anayepiga na kundi la wapiga vyombo bila jina rasmi la bendi.

Onesho hilo mahsusi pia litakuwa maalum katika kuitambulisha taasisi yake aliyoiunda itakayosimamia kazi zake ikiwemo bendi, pamoja na miradi aliyoibuni yenye lengo la kuupromoti muziki wa reggae ili kuhakikisha vijana wengi wanavutika na kujitosa kwenye miondoko hiyo, ili kupanua wigo wa idadi ya wanamuziki wa reggae kwa kuibua vipaji vipya.

Alisema onesho hilo litakalohudhuriwa na wadau wa muziki watakaoalikwa ambao taasisi yake inatarajia kushirikiana nao siku za usoni, litatumika pia kuitambulisha rasmi albamu yake mpya ya nne aliyoirekodia katika studio za Soundcrafters zilizopo Temeke hapa jijini, anayotarajia kuizindua hivi karibuni.
“Katika onesho hilo nitapiga nyimbo zangu zilizonipatia umaarufu miaka ya nyuma ukiwemo wimbo wa ‘Gila’ kutoka albamu ya Money-Pesa (1994), pamoja na nyimbo nyingine kutoka albamu zangu mbili zilizofuata na nyimbo mpya kutoka katika albamu mpya ya ‘Kwa Nini’.”

Utambulisho huo ni mwanzo wa maandalizi ya uzinduzi utakaofuatiwa na ziara ya maonesho yasiyopungua kumi katika awamu ya kwanza, itakayoanzia hapa jijini kabla ya kuelekea nyanda za juu Kusini na baadaye awamu ya pili itahusisha kanda ya Kaskazini na ziwa katika mfululizo wa maonesho ya kupromoti albamu yake mpya na muziki wa reggae kwa ujumla.

Katika onesho la utambulisho atasindikizwa na kundi la Kizazi Kipya cha Reggae, bendi ya Fimbo inayopiga miondoko ya asili, mwimbaji wa muziki wa gospo Mrs Annette Mwasambogo na Dj maarufu wa disco la reggae hapa nchini Aluta Warioba kutoka redio ya Times FM.